๐น TAFAKURI YA MSIBA ๐น
Nimeandika maneno haya kama ushuhuda na kumbukumbu yangu binafsi juu ya ndugu yetu mpendwa Mwalimu Astahili Akilimali aliyefariki jana.
BURIANI KAKA AKILIMALI
Kuondoka kwako kumenifanya niuvunje mwiko niliyojiwekea.
Kwa takriban miezi sita sasa nilinuia โkukaa nyumaโ kwa kujipa likizo ya lazima ya kutoshiriki mijadala wala chochote kwenye makundi sogozi ya Mtandao wa WhatsApp. Sababu nili โ archive magroup yote ili โyasinishughulisheโ! Sababu ya kufanya hivyo ni mada pana inayostahili wakati mwingine wa kuisema kwa upana wake.
Jana jioni, kama vile nilipata โkiherehereโ cha kutamani kusoma ujumbe uliotumwa na Kaka Juma Nchia, nikajikuta nimefungua meseji katika moja ya magrupu ya WhatsApp, mara kwa mshtuko nikapata taarifa ya kuondoka kwako!!!
Nikajiuliza mwenyewe kama alivyojiuliza ndugu yangu Ahmad Juma: โnini kimemsibu Mwalimu Astahili Akilimaliโ?
Mimi nilikwenda mbele zaidi kujiuliza โ aliyefariki ndo huyu huyu Akilimali ninayemjua mimi?
Sijapata majibu na najiona kama naota ninapoandika taโazia hii.
Nilimfahamu kwa mara ya kwanza tulipokutana mara mbili tatu kwenye mikutano ya TAMSA (sasa TAMSIYA) kule katika shule ya Sekondari ya Ununio โ Dar es Salaam miaka ile ya 2000 mwanzoni.
Kipindi hicho vijana wa Kiislamu kupitia jukwaa la TAMSA tulikuwa na ada ya kufanya mikutano yetu kipindi cha mwisho wa mwaka, hususan ile wiki ya mwisho kabisa wakati dunia ikiwa kwenye shamrashamra za Krismasi na Mwaka Mpya.
Ilikuwa wakati wa โkujitambulishaโ mara katokea kijana akiongea kwa ufasaha kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza akitia na vionjo kwa baadhi ya sentensi za Kiarabu kizuri sana.
Tuliohudhuria โkutoka vyuoniโ tukashtuka kidogo. Naona โconfidenceโ yake iko juu, alinidokeza rafiki yangu. Nasi wakati huo tulikuwa na mkakati maalumu wa kuwajengea vijana kujiamini na uwezo wa kuongea mbele za watu (public speaking).
Nilivutiwa sana na uwezo wake na nikamtabiria kwa wenzangu kuwa kijana huyu atakuwa kiongozi mzuri. Sijui kama kaka Omari Msumba, brother Yasin Shamte, Kaka Ahmad Juma na ndugu yangu Abdallah Katunzi wanakumbuka tukio hili.
Maoni ya mmoja wa hao niliowataja yalinifanya wakati wa mapumziko ya kifungua kinywa nimtafute chemba ili tuweze kufahamiana zaidi.
Hivyo ndivyo nilivyopata kumjua Brother Astahili Akilimali. Tulibadilishana mengi na tukawa tukiwasiliana mara kwa mara mpaka nilipomaliza maisha ya kuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa wakati huo.
Nakiri hatukupata kuonana muda mrefu kutokana na ishtighali za maisha, miaka mingi imepita, leo Nchia ananipatia taarifa ambazo zimeninyima usingizi na zaniumiza zaidi kwa kuwa sina hakika kama nitawahi kukusindikiza ndugu yangu Akilimali.
Bado picha ya uso wa bashasha na tabasamu lisilomithilika linafunika kumbukumbu zangu napotamani kukuelezea. Hivi kweli umeondoka!?
Mauti ni fumbo na ukumbusho kwa binaadamu kuwa hayakuwa haya maisha yetu bali ni mchezo na upuuzi.
Nahisi bado niko ndotoni, siamini kama kweli Kamanda umetangulia.
Naikumbuka vema siku ile โniliyokuvamia ofisini kwakoโ, pale katika shule ya Nur โ Magomeni jirani na mwalimu wetu wa Historia Sheikh Mohamed Saidi, nadhani ilikuwa mwaka 2011 au 2012 (sina uhakika โ nina haraka ya kuandika bila hata kuhakiki kumbukumbu zangu).
Nilikuja nikidhani nakuja kumpa โsuprizeโ Mwalimu Saiboko (nae marehemu sasa), tahamaki nikakutana nawe uso kwa uso.
โHivi wewe Mwanaharakati uko hapa, nilidhani nitamkuta kaka Saiboko!?โ Nilingโaka kwa mshangao ukinikaribisha ofisini kwako.
Kama kawaida mapokezi hayo yaligubikwa na tabasamu lisilokwisha. Tuliongea mengi na ukanisaidia fikra ya kumsaidia kijana mmoja kupata nafasi ya kwenda kusoma nje.
Kijana huyo simtaji jina lakini baba yake pia amefariki, ambaye kwa wakati huo alinipa dhamana ya kumlea kwa muda. Ulishiriki katika malezi yale kwa kufanikisha mtoto yule kwenda ngโambo kusoma! Jazakallahu khair.
Si hivyo tu, Mwalimu Akilimali bado uko katika makavazi ya historia ya ujana wangu.
Nakumbuka wakati wa harakati ya kuanzisha Taasisi ya Maendeleo ya Waislamu (MDF) na Mradi wa Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro (MUM) (kwa lugha ya vijana) โulinipa shavuโ la kutosha.
Ilikuwa usiku wa kuamkia UZINDUZI tarehe 22 Mei, 2004 ambapo tulikesha pamoja katika ukumbi wa Diamond Jubilee DSM kufanya maandalizi ya hafla hiyo kuu katika historia ya Waislamu na Elimu Tanzania.
Ulikuwa miongoni mwa vijana wengi waliotuunga mkono kufanikisha maandalizi yale wakati โwanaharakati wengineโ walikuwa wakiipinga juhudi ile.
Kisa? Walikuwa bado hawaamini kama Rais wa wakati huo anaweza kufanya โmema kwa Waislamuโ kutokana na uadui uliokuwepo kwa wanaokumbuka siasa za wakati huo.
Lakini wewe ulijitambua na kunipatia maneno mengi ya faraja kwa โuaduiโ niliokuwa nafanyiwa na baadhi ya watu kwa kuwa kwangu mtendaji wa taasisi ile iliyowezesha hayo.
Wengi hawajui mkasa huo lakini itoshe kusema kaka Akilimali ulisimama upande wa wale wachache (ambao baadae walikuwa wengi) waliokubali โkusimama kando ili wahesabiwe.
Wengi wa waliotupinga kipindi hicho; hivi sasa ni wanufaika wakubwa wa โmazao ya Muslim University of Morogoro (MUM).
Hivyo ndivyo maisha yalivyo. Tusikate tamaa na tushindane kutenda mema. Malipo ni kwa Mola Mlezi wa wote na vyote vilivyomo mbinguni na ardhini.
Uislam wako wa vitendo na kujituma kwako kuliniathiri sana kiwango ambacho nakumbuka nilifikia kukupendekeza uwe โmrithi wanguโ ushikilie kiti nilichokuwa nakalia kipindi hicho.
Nilipendekeza jina lako kwa Marehemu Mzee Kitwana Kondo ambaye pia alikubali wewe ushikilie ofisi ya MDF mwaka 2007 mwishoni nilipopata nafasi ya kwenda kujiendeleza kielimu nje ya nchi.
Bila kusita na kwa uwazi kabisa ulikubali kunirithi kiti kile ambacho wakati wa โurithiโ ulikuwa wakati mgumu kwa kuwa ofisi ile haikuwa na hela wala mshahara. Na fitina zilikuwa bado zinaendelea. Wengi walikuwa hawaamini kile tunachowaeleze kuhusu mustakbali wa Chuo na hali ilivyokuwa wakati huo. Walidhani kuna โmahela yakumwaga ila tunaficha ficha tuโ
Nilikwambia kwa uwazi kwamba โwazee wanguโ hawajanilipa mshahara takriban miezi sita lakini bado ulikuwa tayari kwa hilo. Ni wangapi leo wanaweza kuwa na ari hiyo? Kazi bila posho, thubutu!!!
Huu ndo Uislamu ulionionesha kwa vitendo. Vidole vyangu vinakufa ganzi kwa kutaka kucharaza mengi yanayonipitikia kichwani baada ya kupata taarifa ya msiba huo.
Najaribu kupambana na hali yangu ili nipate muda wa kuja kukuzika ndugu yangu, lakini bado nimeshughulishwa sana.
Ikitokea sijakuwahi kukusindikiza Kisutu, basi pokea salaam na dua zangu za dhati.
Mola akusamehe madhambi yako, na akufanyie wepesi hesabu zako ili kwa ridhaa yake akukutanishe na waja wema katika pepo yake. Aamyn!!
Tangulia Kamanda, tuko nyuma yako.
Msomaji wangu, tuchape kazi na tumtegemee Mola tu. Maisha haya ya Dunia yana nini zaidi ya kula, kunywa na kufurahi!? Kazi na Daโawa.
โSisi sote ni wa Mwenyezi Mungu na Kwake tunarejea.โ
Nduguyo,
SHUKURU MOHAMMED
๐ 11.30am โ 22nd September, 2025