TAARIFA YA MAHAFALI YA TAMSYA WILAYA YA ROMBO - KILIMANJARO
Kwa fadhila na rehema za Mwenyezi Mungu, leo tarehe 05 Oktoba 2025, limefanyika tamasha la mahafali ya wanafunzi wa Kiislamu (TAMSYA) kutoka shule mbalimbali za wilaya ya Rombo. Hafla hii imefanyika katika ukumbi wa Shauritanga Hall na kuhudhuriwa na washiriki kutoka shule 15 zilizopo ndani ya wilaya hiyo.
Mgeni rasmi katika hafla hii alikuwa Br. Abdulrahim Mlulu, ambaye aliwasilisha hotuba ya hamasa iliyojaa mawaidha kwa wanafunzi wahitimu kuhusu umuhimu wa elimu, maadili mema na kuwajibika kama vijana wa Kiislamu.
Aidha, hafla hii ilipata heshima ya kuhudhuriwa pia na
Kaimu Afisa Elimu Sekondari Wilaya ya Rombo, Bi. Mwajuma Rajabu Saguti, ambaye alitoa salamu za pongezi na kusisitiza ushirikiano baina ya uongozi wa TAMSYA na ofisi ya elimu katika kuhakikisha vijana wanapata elimu bora sambamba na malezi ya kiroho.
Katibu wa TAMSYA Mkoa wa Kilimanjaro, Br. Abdulkareem Nzogera, alitoa taarifa ya mwenendo wa TAMSYA, changamoto na mafanikio yaliyopatikana kwa kipindi cha mwaka, huku akiwapongeza viongozi wa wilaya ya Rombo kwa kuandaa mahafali haya kwa weledi mkubwa.
Sheikh wa Wilaya ya Rombo aliongoza dua ya pamoja kuwaombea wahitimu mafanikio, kuimarika kwa umoja wa wanafunzi wa Kiislamu na kuendelea kwa jitihada za TAMSYA katika maeneo yote ya mkoa wa Kilimanjaro.
Tunaomba Mwenyezi Mungu aendelee kuwaongoza wahitimu wetu katika mitihani na maisha yao, na awalipe kheri wale wote waliochangia kufanikisha tukio hili muhimu.
Imetolewa na:
Br. Abdulkareem Nzogera
Katibu TAMSYA Mkoa wa Kilimanjaro*
Tarehe: 05/10/2025
Eneo: Shauritanga Hall
Wilaya ya Rombo